| dc.description.abstract |
Utafiti huu unachunguza nduni mahsusi za kimtindo zinazotumiwa na waandishi wa
riwaya teule za Kiswahili kusawiri maudhui ya dini na mamlaka. Riwaya zilizoteuliwa
ni: Paradiso (2005) ya John Hamu Habwe, Nguvu ya Sala (1999) ya Kyallo Wadi
Wamitila , Asali Chungu (1978) ya Said Ahmed Mohamed, pamoja na Kasri ya Mwinyi
Fuad (1978) ya Shafi Adam Shafi. Ingawa kijuujuu riwaya hizi zinachunguza maudhui
ya dini na mamlaka, kiundani zinachunguza masuala kama vile jinsia, ukosefu wa ajira
miongoni mwa vijana, uhalifu mijini, umaskini, ufisadi, tamaa ya pesa na mali, na
ukandamizaji. Haya ni masuala ibuka ambayo waandishi wa riwaya teule
wanayaangazia kwa mtazamo wa dini na mamlaka. Mkabala wa kimtindo haujatumika
sana kuchunguza masuala ibuka kama haya katika riwaya ya Kiswahili. Uchunguzi huu
uliongozwa na malengo yafuatayo: kufafanua jinsi uteuzi wa kileksika unavyojitokeza
kama nduni ya kimtindo katika kuchimuza masuala ya dini na mamlaka katika riwaya
teule. Kuchanganua matumizi ya nduni za kisintaksia katika kuchimuza maudhui ya
dini na mamlaka katika riwaya teule. Kuhakiki matumizi ya tamathali za usemi kama
mbinu za kimtindo katika uchimuzi wa masuala ya dini na mamlaka
katika riwaya teule. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchimuzi. Uchanganuzi wa
data uliongozwa na mihimili ya Nadharia ya Uchimuzi: ukiushi na usambamba. Utafiti
huu ni wa kitaamuli na tulitumia muundo wa usanifu kifani. Mkabala wa kitaamuli
ulitumiwa kwa sababu utafiti huu unazingatia fasiri ya ruwaza za nduni mahsusi za
kiisimu, mintarafu ya masuala ya dini na mamlaka. Tena, tulizingatia mfumo wa
kifalsafa wa kiufasiri. Data ilikusanywa kutoka riwaya nne za Kiswahili ambazo
ziliteuliwa kimaksudi. Mahitimisho ya utafiti yaliwasilishwa kidhamira. Kuhusu lengo
la kwanza, utafiti huu uligundua kwamba visawe na urudiaji ndiyo mikakati ya
kileksika iliyotumiwa zaidi na waandishi kuibua masuala ya dini na mamlaka katika
riwaya teule. Kuhusu lengo la pili, iligundulika kwamba anafora na usambamba wa
kiusawe ndizo mbinu za kiusambamba zilizotumika zaidi katika riwaya teule. Aina
nyingine za usambamba zilizotumiwa ni pamoja na epifora, tanakuzi, na mgeuko wa
polepole. Kuhusu lengo la tatu, tamathali ya usemi iliyotumiwa zaidi kuchimuza
maudhui ya dini na mamlaka ni sitiari. Hata hivyo, mbinu za tashbihi, kinaya na kejeli
pia zilitumika sana katika riwaya zote zilizochanganuliwa. Kwa jumla, inadhihirika
kwamba mamlaka yana dhima muhimu sana katika maisha ya wanajamii kwa vile
yamefumwa katika mfumo wao wa kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Utafiti huu
unaonyesha kwamba waandishi wanadhamiria kujenga maudhui kuhusu masuala ya
dini na mamlaka na wanatumia mbinu zinazoonyesha jinsi ambavyo matini zinajadili
masuala ya muhimu katika jamii zinazosawiriwa. Utafiti huu unasisitiza haja ya
kuziangalia matini kama mazao ya jamii husika zinazosawiriwa. Unabainisha utaratibu
wa kuzichanganua riwaya za Kiswahili kwa kuzingatia ngazi za kileksika, kisarufi na
kisemantiki. Utafiti huu unapendekeza tafiti nyingine za kimtindo zifanywe kwa
kuzingatia nadharia nyingine kuchunguza masuala ya dini na mamlaka. Pia akili unde
ihusishwe katika utafiti wa kimtindo. |
en_US |