| dc.description.abstract |
Nyimbo za kiasili ni maarufu sana miongoni mwa jamii ya Wakamba. Nyimbo hizi
huimbwa katika kila hafla ya kijamii na husheheni itikadi ya Wakamba kuhusiana na
masuala mbalimbali. Hata hivyo, itikadi katika nyimbo hizi za kiasili hufumbatwa
kijazanda. Azma ya utafiti huu ni kuchunguza iwapo kuna uhusiano baina ya jazanda
zinazotumika katika nyimbo za kiasili za Kikamba na itikadi ya jamii ya Wakamba.
Malengo maalum ya utafiti ni matatu. Kwanza, ni kupambanua jazanda mahsusi
katika nyimbo za kiasili za Kikamba zinazowasilishwa kwenye hafla maalum. Pili,
kuhakiki itikadi za Wakamba zinazofumbatwa kijazanda kwenye nyimbo hizo za
kiasili. Tatu, kutathmini uamilifu wa jazanda mahsusi kifani na kimaudhui kwenye
nyimbo za kiasili za Kikamba. Utafiti huu umechukua muundo wa kithamano ambapo
nyimbo za kiasili za Kikamba zimehakikiwa na kufasiriwa kwa kuzingatia muktadha
wa kijamii ambamo nyimbo hizo zinaimbwa na kupokelewa. Data ya kimsingi
ilitokana na nyimbo za kiasili za Kikamba zilizokusanywa kutoka Kamisheni ya
kudumu ya Muziki ya Rais (PPMC) nchini Kenya. Nyimbo zilizosheheni jazanda
zilisampuliwa kimakusudi, zikatafsiriwa kutoka Kikamba hadi Kiswahili na
kuchanganuliwa. Uchanganuzi wa data uliegemezwa kwenye malengo ya utafiti na
mihimili ya kinadharia. Nadharia ya Jazanda Dhanifu kwa mujibu wa Lakoff na
Johnson na Nadharia ya Itikadi ilivyofafanulliwa na Van Dijk ndizo msingi wa utafiti
huu. Nadharia ya Jazanda Dhanifu ilielekeza uhakiki wa itikadi zilizofumbatwa
kijazanda na uamilifu wa jazanda hizo kifani na kimaudhui katika nyimbo za kiasili
za Kikamba. Nadharia ya Itikadi nayo ilitumika kupambanua maumbo ya kimsingi ya
utambuzi wa kijamii yalivyodhihirika katika hafla za kijamii ambamo nyimbo za
kiasili za Kikamba hutokea. Matokeo ya utafiti yameonyesha kuwa jazanda katika
nyimbo za kiasili za Kikamba huambatana na hafla mahsusi za kijamii. Nyimbo hizi
za kiasili husheheni jazanda ambazo hufumbata mwonoulimwengu, mielekeo na
maadili ya jamii ya Wakamba kuhusiana na masuala kama vile; siasa na uongozi,
ndoa na malezi, uchumi na uwajibikaji. Tunaweza kuhitimisha kuwa jazanda katika
nyimbo za kiasili za Kikamba ni nyenzo muhimu ya kuwasilisha itikadi ya Wakamba
kwa hadhira lengwa. Jazanda hizi zinajidhihirisha kama nguzo kuu ya kuwasilisha
imani, maadili na mienendo ya Wakamba. Kwa hivyo, kimaudhui, jazanda
zinazotumika katika nyimbo hizi za kiasili zinakuza na kuthabitisha akilini mwa
hadhira ujumbe unaowasilishwa kitaswira. Kifani, jazanda zinasafidi lugha
inayotumiwa kimafumbo katika nyimbo za kiasili na kwa njia hii kupunguza makali
kihisia miongoni mwa hadhira. Aidha, utafiti umeonyesha kuwa matumizi ya jazanda
katika nyimbo za kiasili za Kikamba huibua picha ya dhana zinazorejelewa akilini
mwa hadhira na hivyo kuimarisha kumbukumbu ya virejelewa na burudani.
Kitaaluma, matokeo ya utafiti huu ni muhimu kwa vile yatakuza maarifa kuhusiana
na uamilifu wa nyimbo za kiasili za Kikamba na fasihi simulizi ya jamii za Kiafrika
kwa ujumla. Kijamii, utafiti ni hatua mojawapo ya kuhifadhi utamaduni na
utambulisho wa jamii ya Wakamba. Kiuchumi, ni kichocheo kwa wasanii wa nyimbo
za kiasili kutumia vipawa vyao kujipatia riziki. Kwa hivyo, utafiti huu unapendekeza
kutekelezwa kwa Mwongozo wa Sera ya Kitaifa ya Muziki unaopendekeza
wanamuziki na wasanii kwa ujumla wanufaike kikamilifu kutokana na kazi zao za
kisanaa. |
en_US |