| dc.description.abstract |
Utafiti huu ulichunguza matumizi ya lugha na mikakati ya mawasiliano katika
mandhari ya lugha mjini Eldoret. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kubainisha
maudhui mbali mbali na mzagao wao katika mabango,kutathmini kwendana kwa
uteuzi wa lugha kwa matarajio ya hadhira lengwa na kuchunguza ufaafu wa vielelezo
vya mabango kama mikakati ya kuwasilisha ujumbe kwa hadhira lengwa. Utafiti huu
ulijikita katika madai ya nadharia ya lugha-tarajiwa na isiyotarajiwa, baadhi ya madai
ya nadharia ya lugha-solo na lugha-bebwa na nadharia ya semiotiki. Data za utafiti
huu zilikusanywa katika barabara mbili kuu zilizoteuliwa kimakusudi mjini Eldoret;
barabara ya Oginga Odinga na barabara ya Uganda. Makundi manne ya vijana na
wazee yalihojiwa na kurekodiwa katikati mwa mji wa Eldoret. Usampulishaji kusudio
ulitumika. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha maudhui mbali mbali na mzagao
wao; benki (9.79%), elimu (1.39%), vinywaji (17.48%), bima (1.39%), uganga
(0.69%), ajira (0.69%), vyakula (6.99%), Kamari (0.69%), habari na mawalisiano
(18.88%), fenicha (0.69%), kilimo (9.09%), uchukuzi (9.09%), michezo (0.69%),
bidhaa jumla (14.68%), matibabu (2.79%) na kongamano (2.79%). Pia, tuligundua
ruwaza nne za uteuzi wa lugha; Kiingereza (49.65%), ubadilishaji msimbo (32.86%),
Kiswahili (14.68%) na Kinandi (2.69%). Hatimaye, utafiti huu ulibainisha kuwa,
uteuzi wa ujozi lugha katika mabango hayakuendana na matarajio ya hadhira. Hata
hivyo, utafiti huu uling`amua kuwa matumizi ya viziada lugha kama vile picha, rangi
na fonti mbali mbali hushadidisha mawasiliano katika matangazo ya mabango.
Tasnifu hii inapendekeza kuwa, kwa kuwa mandhari ya lugha mjini Eldoret
yameonyesha ubadilishaji msimbo na lugha zisizo thabiti za Sheng na Engsh huku
lugha ya asili ya eneo la mji wa Eldoret, Kinandi, ikitumika kwa uchache sana.
Ukweli ni kwamba haiwezekani kujumlisha hali ya mandhari ya lugha nchini Kenya
kwa kujikita katika mji mmoja tu. Kwa hivyo, tunapendekeza utafiti zaidi uendeshwe
katika miji mingine. |
en_US |